Tuzo za Usuluhishi kwa Mwaka 2024
Mpendwa Mwanachama,
Salaam,
Tunapenda kukufahamisha kuwa, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro (TIAC) tumepokea barua ya mualiko ya kushiriki Tuzo za Usuluhishi kwa Mwaka 2024 zilizoandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzaniakupitia Mahakama Kuu kituo cha Usuluhishi. Tuzo hizo zina lengo la kutambua mchango wa wadau katika kuwezesha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro ikijumuisha njia za Usuluhishi (Arbitration), Upatanishi (Mediation), Kurudisha Mahusiano ya Kirafiki (Reconciliation) na Mazungumzo kufikia Makubaliano (Negotiation).
Hii ni moja ya mikakati ya Mahakama ya Tanzania katika kukuza na kuhamasisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro, njia ambazo zinakubalika duniani kote kwa kuwa na faida nyingi katika utatuzi wa migogoro inayojitokelza katika jamii zetu pamoja na kuepusha gharama za uendeshaji wa mashauri kupitia taratibu za kimahakama.
Tuzo hizo zilianza rasmi mwaka jana kwa mkoa wa Dar es Salaam na kufanyika kwa mafanikio makubwa, hivyo Mahakama kuu ya Tanzania imeweka utaratibu wa kutolewa kwa tuzo hizo kila mwaka kwa makundi tofauti tofauti. Kwa kuzingatia hayo, vifuatavyo ni vigezo vilivyoandaliwa na Mahakama kuu Kituo cha Usuluhishi vitakavyotumika katika utoaji wa tuzo hizo:
Vigezo kwa Mawakili wa Kujitegemea (Wanachama wa TLS):
- Idadi na aina ya Migogoro aliyoshiriki katika hatua ya Usuluhishi nje na ndani ya Mahakama
- Madai ya Migogoro
- Migogoro iliyofanikiwa kupitia njia za Usuluhishi
- Wadaawa waliohusika
- Muda uliotumika kwenye Usuluhishi
- Gharama zilitotumika kwenye Usuluhishi
- Idadi ya Mashauri yaliosuluhishwa bila kufika mahakamani
- Maslahi kwa Umma yanayotokana na Usuluhishi
- Eleza namna mgogoro ulivyomalizika (Yasizidi maneno 50)
Vigezo kwa Wasuluhishi Binafsi – Kupitia Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro (TIAC):
- Idadi ya Migogoro iliyopokelewa kwa ajili ya Usuluhishi
- Aina ya Migogoro
- Madai ya Mgogoro unaobishaniwa
- Wadaawa waliohusika
- Migogoro iliyofanikiwa kupitia njia za Usuluhishi
- Gharama zilizotumika kwenye Usuluhishi
- Makubaliano yaliofikiwa na Uhusiano ulioboreshwa
- Maslahi kwa Umma yanayotokana na Usuluhishi
- Eleza namna mgogoro ulivyomalizika (Yasizidi maneno 50)
Maombi yote yatumwe kwenda kwa Naibu Msajili Mahakama Kuu Usuluhishi kupitia barua pepe ya ofisi mediationcentre@judiciary.go.tz na nakala kwa (cc) Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwenda rsalvatory@tls.or.tz na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro (TIAC) kwenda info@tiac.or.tz , muda wa kuwasilisha maombi ni tarehe 30 Juni na 15 Disemba 2024.
Kwa ufafanuzi na maelekezo zaidi tafadhali wasiliana na Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kituo cha Usuluhishi kupitia nambari ya simu ya mkononi 0719 538868.
Regards,
|Tanganyika Law Society Secretariat
2 Replies to “Tuzo za Usuluhishi kwa Mwaka 2024”
Habari, Tunashida kubwa ya kuzulumiwa shamba letu lililopo Chanika wilaya ya Ilala DSM.Naomba kama inawezekana mtusimamie au mtupe ushauri tufanyaje ili tupate haki yetu.Asante.
Asante kwa kutemebelea tovuti yetu. Tunazo ofisi zetu wilaya ya Ilala na mawakili wa kukupa msaada wa kisheria. Tafadhali tupatie mawasiliano yako (Namba ya simu)ili tuweze kukunganisha nao. andelea kufatilia TLS kupitia tovuti yetu na mitandao ya kijamii ikiwemo Wakili TV kuwa ajili ya elimu ya sheria katika lugha nyepesi.