TAMKO NA RAI YA TLS KWA UMMA JUU YA MBINU ZA KUPAMBANA NA UGONJWA WA KORONA

Ndugu Watanzania,

Mnamo tarehe 16 Machi 2020, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kupitia kwa Waziri wa Afya, Jinsia na Watoto, Mh Ummy Mwalimu, ilitangaza kuingia nchini kwa ugonjwa wa virusi vya korona baada ya mgonjwa mmoja kugundulika mkoani Arusha. Hadi Jumamosi ya tarehe 18 Aprili 2020 wagonjwa 147 wamegundulika nchini, huku watano kati yao wakipoteza maisha. Kwa hiyo ndani ya mwezi mmoja tu idadi ya wagonjwa imeongezeka kwa kiwango kikubwa sana kwa vipimo vya asilimia. Siku moja tu, baadae, yaani tarehe 17 Machi 2020 Waziri Mkuu aliamuru kufungwa kwa shule zote nchini na baada ya siku chache amri hii ilivikumba vyuo vyote ambavyo wanafunzi wake walikuwa likizo.

Sambamba na kufungwa kwa vyuo, Serikali ilizuia mikutano na mikusanyiko ya watu wengi katika sehemu mbalimbali isipokuwa misiba na ibada za kidini. Aidha, ilitaka usafiri wa umma uzingatie uwezo wa upakiaji wa kila gari na hivyo kuzuia upakiaji wa abiria zaidi ya idadi ya viti vya kuketi katika gari.  Haikuishia hapo, ikataka wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, na kunawa mikono yao kwa sabuni na vitakasaji, na kutumia vichuja pumzi (masks/barakoa) ili kuzuia maambukizi kati ya mgonjwa na yule asiye na ugonjwa. Hatua nyingine ni kuepuka mbanano wa watu popote pale walipo na hivyo kuhakikisha umbali-jamii  wa walau mita moja na nusu kati ya mtu na mtu.

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeutangaza ugonjwa wa virusi vya korona maarufu kama COVID-19, kuwa ni baa la dunia.  Tangazo hilo linaaminisha kuwa nchi zote duniani ni waathirika wa ugonjwa huo na kuwa mikakati na juhudi za pamoja lazima zielekezwe kupambana na ugonjwa huo. Hadi tarehe 18 Aprili 2020 idadi ya wagonjwa wa ugonjwa huu duniani ni 2,258,909 na vifo ni 154,388 huku Marekani, Italia, Hispania na Uingereza zikiwa ndizo zinazoongoza kwa idadi ya wagonjwa na vifo.

Licha ya kuwa ugonjwa huu umezikumba karibu nchi zote duniani, nchi ambazo zilichukua hatua kamili zisizo na mlegezo wowote hivi sasa zimeweza kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu. Nchi hizo ni Korea ya Kusini, Ujerumani, Denmark, Norway, na hata majirani zetu wa Uganda na Rwanda. Korea-Kusini na Ujerumani ziliweka mkazo katika zuio la watu kutoka nje na upimaji wa watu kwa idadi kubwa ili kubaini walioambukizwa na kuweza kuwatoa katika jamii, kuwafahamu wale waliokutana nao, na kuweza kuwatibu. Aidha, Korea Kusini iliwataka wananchi wake kuvaa vichuja pumzi muda wote wanapokuwa wametoka nje. Ujerumani nayo iliwekeza sana katika kupima watu, kuwabaini wagonjwa, kuwapeleka wagonjwa katika hospitali maalumu na kuwapatia matibabu. Nchi za Italia, Hispania, na Marekani kwa upande mwingine zilichelewa kuchukua hatua kamili za kuzuia mikusanyiko ya watu, sherehe, na huduma za maisha ya kawaida. Zilikuja kuzinduka na kuweka mazuio makali wakati ugonjwa umeingia na kusambaa sana na hivyo hatua walizochukua ni za kuchelewa ambazo zilikuwa ni za kupambana na moto wa gesi. Madhara ya kuchelewa yamesababisha watu wengi kupoteza maisha yao na kuparaganyika kwa chumi zao.  Marekani ambayo hadi tarehe 20 Januari 2020 ilikuwa na mgonjwa mmoja sasa ina wagonjwa 759,786 na zaidi ya vifo 40,683.

TLS kwa kutambua wajibu wake wa kisheria chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Chama cha Sheria cha Tanganyika (Tanganyika Law Society Act) kinachoipa majukumu ya kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali, Bunge, Mahakama na umma, na kuongozwa na jukumu azizi ambalo kila mwananchi wa Tanzania analo chini ya Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isemayo: “14. Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.”, inapenda kutoa ushauri huu kwa wadau wake wote yaani Serikali, Bunge, Mahakama, na watu wote waishio nchini Tanzania:

a. Kuwekwa marufuku ya mikusanyiko ya watu katika sehemu mbambali ikiwa ni pamoja kwenye baa, sherehe za harusi na za kijamii, mikutano ya viongozi wa Serikali isipokuwa ya kiutendaji ya kamati maalumu za kupambana na baa la ugonjwa wa korona. Ieleweke kuwa zuio hili halitagusa watu wa sekta za afya, ulinzi na usalama, bandari na usafirishaji wa bidhaa zinazotakiwa kutumika nchini na nje ya nchi. Ila wafanyakazi wote hawa lazima wapewe vifaa vya kujikinga na maambukizi;

b. Kuweka utaratibu mzuri wa watu kuingia na kutoka masokoni kujipatia mahitaji yao ikiwa ni pamoja na kuanzisha masoko-mitaa katika siku maalumu za wiki kwa watu kujipatia mahitaji yao ya msingi;

c. Kuwekwa karantini ya watu wote kutoka nje ya nyumba zao kwa muda wa siku 21 nchini kote ili kuweza kuzuia kuendelea kusambaa kwa ugonjwa huu nchini hii ni kuongozwa na kanuni ya kuzuia (precautionary principle) au kuzuia ni bora kuliko tiba ambayo ni kanuni ya 15 ya Azimio la Rio na ni moja ya kanuni za msingi za ulinzi wa mazingira na afya ya watu zilizoanishwa na kifungu cha 7(3)(c) cha Sheria ya Utunzaji Mazingira ya Mwaka 2004 na vifungu 4(1)(a)-(d), 9(2) na 12(1) vya Sheria ya Afya Jamii Namba 1 ya Mwaka 2009 pamoja na Kanuni za Kimataifa za Afya za Mwaka 2005 ambazo ni sehemu ya Sheria ya Afya Jamii ya Mwaka 2009;

d. Kuhakikisha kuwa madaktari, wauguzi na wote wanawahudumia wagonjwa wa virusi vya korona wanapewa nguo na vifaa vya kutosha vya kujikinga na maambukizi;

e. Kwa kuwa mfungo wa Ramadhani unatarajiwa kuanza wiki hii, Serikali iweke mkazo wa kuhakikisha kuwa vyakula vya muhimu vitakiwavyo vinapatikana kwa bei nafuu na kuuzwa kwa utaratibu mzuri ambao utazuia maambukizi;

f. Sambamba na zuio la aina ya karantini usafiri wa umma na binafsi upigwe marufuku kwa muda wa siku 21 ili kuweza kuzuia kusambazwa kwa ugonjwa huu;

g. Kuanzishwa kwa mkakati maalumu wa kupima watu nchini ili kuweza kuwabaini watu ambao wameambukizwa ambao wanajijua au wasiojijua kama zilivyofanya na zinavyofanya nchi za Korea Kusini, Ujerumani, na hata majirani zetu wa Rwanda, Kenya na Uganda,

h. Kunyunyizia dawa katika miji na mitaa mbalimbali hapa nchini ili kuua virusi wa ugonjwa wa korona,

i. Kutoa msamaha wa kulipa mikopo na marejesho ya malipo ya mikopo kwa muda wa miezi mitatu kwa watu waliokopa kutoka taasisi za fedha nchini;

j. Serikali kuhakikisha kuwa vifaa vya kujikinga na ugonjwa huu vinagawiwa na kusambazwa kwa wananchi bure au kwa bei nafuu kabisa huku Mamlaka za Maji zikiweka kiwango cha maji ambacho hakitatozwa tozo za kila mwezi kama njia ya kukabiliana na ugonjwa huu;

k. Serikali kuandaa na kutekeleza mkakati maalumu wa kuziokoa sekta za kiuchumi nchini ambazo zimeathiriwa kutokana na baa la ugonjwa huu;

l. Benki kuweka mkakati wa makusudi kuirejea na kuihusha mikataba ya mikopo kutokana na wakopaji wao kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na baa hili kwa kutumia kanuni ya nguvu isiyohimilika (farce majeure);

m. Aidha, kuzuia kutozwa kodi ya pango kwa waajiri na wafanya biashara kwa kipindi cha miezi mitatu kama njia ya kutoa nafuu kwa waajiri na wafanya biashara kutokana na mdororo mkubwa wa uchumi uliosababishwa na baa la ugonjwa wa korona;

n. Kusamehewa kulipa kodi kwa kipindi cha miezi mitatu kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa wafanya biashara na waajiri ambao shughuli zao zimeathiwa na ugonjwa huu;

o. Kuanzishwa kwa mpango maalumu wa kugawa na kusambaza vyakula kwa familia zenye uwezo mdogo wakati wote wa kipindi cha karantini ya siku 21;

p. Kuboreshwa kwa mfumo wa afya jamii ili kuwezesha kukabiliana na milipuko ya pili na ya tatu ya ugonjwa huu kwani kwa mujibu wa historia ya mabaa ya magonjwa ya maangamizi kama huu wa korona, mlipuko wa kwanza hufuatiwa na milipuko mingine ya pili na ya tatu;

q. Kuheshimu bila kuyumba au kejeli umuhimu wa kutunza na kulinda mazingira nchini ikiwa ni pamoja na sheria za mipango mijini, na afya jamii;

r. Serikali iombe msaada kutoka taasisi za kidunia na nchi kupata rasilimali fedha za kupambana na baa hili pamoja na kusamehewa kulipa madeni yake kutokana na uchumu wake kuathiriwa kwa baa hili;

s. Waajiri kuweka utaratibu wa wafanyakazi wao kufanya kazi wakiwa nyumbani kwa shughuli zile ambazo zinaweza kufanywa wafanyakazi wakiwa nyumbani ili kupunguza kuparaganyika kwa uchumi nchini;

t. Kufuatwa na kuheshimiwa kwa Sheria ya Afya Jamii Namba 1 ya Mwaka 2009 ambayo imeanisha madaraka ya Waziri, Maafisa Afya wa Mikoa na Wilaya pamoja na mamlaka ya kuwaweka wagonjwa karantini;

u. Kurekebisha Sheria ya Afya Jamii na kutoa Mamlaka kwa Waziri wa Afya kutangaza kwa baa au janga la ugonjwa wa maangamizi, maambukizi na mlipuko wa kitaifa na kimataifa na hatua zinazotakiwa kufuatwa na kila mwananchi katika eneo husika ili kuzuia au kukabiliana na baa hilo;

v. Wananchi watumie tiba za asili zinazofahamika za kupambana na magonjwa ya maambukizi ya hewa kama sehemu ya kujikinga na kujiepusha na ugonjwa huu bila kuacha kufuata mashariti ya wataalamu wa afya;

w. Kuboreshwa kwa Sheria ya Afya Jamii Namba 1 ya Mwaka 2009 ili kuunda taasisi ya kitaifa ya kushughulikia magonjwa ya mlipuko, maambukizi, na maangamizi na kuratibu utendaji wa kazi za afya jamii zinazofanywa na Serikali za mitaa. Aidha, sheria iweke mkazo wa kutengwa na kupewa rasilimali fedha na watu kwa taasisi zinazohusika na masuala ya afya jamii na kinga dhidi ya utendaji kugeuzwa mchezo wa kisiasa;

x. Kuondolewa magerezani mahabusu ambao makosa yao yanadhaminika na wale ambao walizuiwa kupewa dhamana kutokana na Mkurugenzi wa Mashitaka kuweka hati ya kuzuiwa dhamana zao;

y. Kutolewa msamaha wa Raisi kwa wafungwa ambao wanakaribia kumaliza muda wao na wale ambao makosa yao si ya mauaji, ubakaji, wizi wa kutumia nguvu, na dawa za kulevya kama heroini.

z. Mahakama kuahirisha kusikilizwa kwa kesi kwa kipindi cha siku 30 na kuendelea kusikiliza kesi zile tu ambazo zaweza kusikilizwa kwa njia ya mtandao wa video huku usalama wa mahakimu, majaji, mashahidi na wadaawa ukihakikishwa.

aa. Viongozi wa kidini wachukue hatua madhubuti za kuanza kuendesha ibada na sala zao kwa njia ya redio na mitandao ili kuondoa uwezekano wa kuambukizana;

bb. Watu wote wasali kwa unyofu mkubwa sana kwa Mungu wetu mwema ili atuokoe na baa hili sisi sote hapa nchini na duniani kote;

cc. Baa hili liwe funzo kwa dunia nzima kuwa mifumo ya nchi zote duniani ya afya ina upungufu mkubwa licha ya tofauti zetu za kiuchumi. Ni lazima nchi zote zishirikiane kuweza kuboresha mifumo yao ya afya. Kwa upande wetu hapa nchini tujue kuwa afya ni mali na hivyo tuwekeze sana katika kuboresha miundomisingi ya afya licha ya uchumi wetu mdogo. Tuige mfano wa Cuba ambayo ina mfumo mzuri sana wa afya licha ya uchumi wake mdogo.

Ni imani ya TLS kuwa hatua tulizopendekeza zitaiwezesha nchi yetu kuushinda ugonjwa huu na kurejea katika maisha yetu ya awali, yaliyobusarishwa na ugonjwa huu, kwa haraka sana. Kama hatua hizi madhubuti hazitachukuliwa ni wazi kuwa shule na vyuo havitafunguliwa, michezo na shughuli za kawaida zitaendelea kufungwa kwa kipindi chote cha mwaka huu kwani kila siku idadi ya wagonjwa itazidi kuongezeka na hivyo kuwa katika mazingira magumu kabisa. Kuendelea kuwepo kwa ugonjwa kwa muda mrefu kutakuwa na athari kubwa sana za kiuchumi sana kwani mataifa mengine ambayo yatakuwa yamekwisha utokomeza ugonjwa huu, yatakataza raia wao kuja nchini na raia wetu watakatazwa kwenda katika nchi hizo na hivyo nchi yetu kupoteza fursa nyingi sana za kiuchumi tukitaja tu sekta ya utalii.

TLS inawataka Watanzania na watu wote wanaoishi nchini kutoufanyia mzaha ugonjwa huu wa korona na wafuate kwa umakini maagizo ya wataalamu wa afya. Wananchi tuache mikusanyiko, tukae majumbani mwetu, tutoke nje tu kuhemea mahitaji ya muhimu, tuwafundishe watoto wetu, tutiane moyo, na kusali kwa Mungu wetu bila kuchoka. TLS inaamini kuwa Mungu wetu mwema atasikiliza sala zetu pale ambapo tumefanya majuto ya kweli, tumeacha njia zetu mbaya, tumewabaini wagonjwa wa ugonjwa huu, tumewagundua walioaambukizwa ila si wagonjwa, na kuzuia kuendelea kwa maambukizo. Tusitegemee miujiza kutoka kwa Mungu bila sisi kufanya kila tutakiwacho kwa akili tulizokirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Imetolewa kwa mamlaka ya Baraza la Uongozi wa TLS Jijini Dar es Salaam leo tarehe 20 Aprili 2020

Dkt. Rugemeleza A.K. Nshala

Raisi

bofya hapa kupata waraka uliosainiwa ==> https://tls.or.tz/wp-content/uploads/2020/04/WARAKA-WA-TLS-JUU-YA-KORONA.pdf

 

Calendar
August 2022
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031  

Get In Touch

Latest Posts

Shopping Cart

No products in the cart.