Tamko la TLS Juu ya Wimbi la Pili la Mlipuko wa Ugonjwa wa Korona

TAARIFA KWA UMMA

Ndugu Watanzania,

TAMKO LA TLS JUU YA KUWEPO KWA WIMBI LA PILI LA UGONJWA WA KORONA NCHINI

Mnamo tarehe 13 Februari 2021 Baraza la Uongozi la TLS lilikutana kutekeleza majukumu yake na moja ya ajenda ya kikao hicho ilikuwa ni umuhimu wa TLS kuitaka Serikali  kutoa tamko lilinyooka juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa korona na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo nchini. Kama Chama TLS imeguswa sana na vifo vinavyotokana na ugonjwa huu kwani tokea tarehe 1 Januari 2021 hadi tarehe 13 Februari 2021 mawakili 22 walikwishapoteza uhai wao kwa magonjwa mbali mbali ikiwemo ugonjwa wa korona na idadi hiyo imeongezeka na kufikia 25 kufikia tarehe ya leo. Baadhi yao waliandika hata ujumbe wa buriani kwani waligundulika wakati tayari hali zao zikiwa ni mbaya sana. Vivyo hivyo katika mitaa yetu na sehemu za kazi tumeshuhudia watu wakifariki na tumejumuika wa familia za wafiwa na waombolezaji katika misiba na maziko.

TLS inasimamia misingi ya utawala wa sheria nchini na inatakiwa na Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika Sura ya 307 ya Sheria za Tanzania kuishauri Serikali na kuusaidia umma wa Watanzania kuhusiana na masuala mbalimbali yahusuyo haki na sheria. Kwa sababu hiyo tunatambua kwamba viongozi wote waliochaguliwa na wananchi waliapa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo katika Ibara ya 14 inaelekeza ulinzi wa haki ya kuishi na Ibara ya 18(d) inaelezea haki ya raia kupewa taarifa zinazohusu maisha yao kama tunavyonukuu:-

Ibara ya 14:  Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.

Ibara ya 18(d): Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.

TLS imekuwa ikifuatilia kwa makini mwenendo mzima wa mlipuko wa ugonjwa wa Korona tangu Februari Mwaka 2020 na kuona juhudi mbalimbali zilizochukuliwa na wananchi na Serikali katika kupambana na ugonjwa huu uliosababisha vifo vingi ulimwenguni hata kuwa janga kubwa la kimataifa lililoleta mtafaruku dunia nzima.  Msimamo wa TLS ni kwamba, dawa yotote ya kudumu ya tatizo sio kulikanusha tatizo hilo na wala siyo kubeza ukubwa wa tatizo husika bali kukabiliana nalo kwa umakini na utaalamu mkubwa ili kujua chanzo cha tatizo, ukubwa wa tatizo, athari za tatizo na njia/dawa sahihi ya kulitatua au kupambana nalo.

Ikiwa wahusika watakana kuwepo kwa tatizo, wakati lipo, basi haiwezekani kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na tatizo lenyewe. Ikiwa tatizo japo dogo kupuuzwa, ni dhahiri kuwa ukubwa wa tatizo huweza kuongezeka kutoka hali inayoweza kudhibitiwa hadi kufikia hali isiyoweza tena kudhibitiwa. Kwa utamaduni wa Kitanzania na pia kwa nadharia za kitaalamu sote tumefunzwa kuwa ni heri kukinga kuliko kujaribu kuponya. Kwa sababu hiyo, TLS inaaamini kuwa ugonjwa wowote inafaa ushughulikiwe mapema kabisa kwani katika hatua za mwanzo, magonjwa mengi hutibika kirahisi na uwezekano wa kupunguza athari zake mbaya ni mkubwa zaidi.

Mnamo Mwaka 1978, nchi yetu ilikabiliana na janga la ugonjwa wa kipindupindu. Wakati huo, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere   alitumia methali ya Kizanaki isemayo: “Nyambhisabhisa uburweire ekerro keramboora” yaani “mficha ficha maradhi kilio kitamuumbua”. Mwalimu alitumia kauli hiyo kuelezea umuhimu wa uwazi katika mapambano ya maradhi au kukabiliana na tatizo.  TLS inaamini kuwa kuendelea kukanusha kwamba hakuna wagonjwa wa korona nchini Tanzania si sawa, isipokuwa ni kushindwa kutimiza matakwa ya Ibara ya 18(d) ya Katiba. Huko ni kuwanyima wananchi wa Tanzania haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu hali iliyopo na inavoweza kuhatarisha maisha yao. Tunaamini kuwa, ikiwa wananchi watapewa taarifa za ukweli, sahihi na kwa wakati muafaka – basi ni wazi kila mwananchi atajitahidi kuchukua hatua zinazomfaa kujilinda na kuuhifadhi uhai wake na wa wale wanaomtegemea.

Sisi wanachama wa TLS kwa ujumla tunaona na tunasikia wenyewe kila wakati mambo yanayotokea mitaani mwetu na kama ulivyo msemo wa wahenga kwamba “mwenye macho haambiwi tazama.”   Kwa ujumla ndugu zetu na wengi wetu kama Watanzania ni mashuhuda wa wimbi kubwa la vifo katika jamii yetu na huo ndio ukweli na ndiyo maana tunashauri viongozi wa umma na vyombo vya dola kutangaza hadharani kuwepo kwa ugonjwa huu wa korona ili kuondoa sintofahamu inayoukabili umma wetu.

TLS kwa kutambua wajibu wake wa kisheria chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Chama cha Sheria cha Tanganyika (Tanganyika Law Society Act) kinachoipa majukumu ya kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali, Bunge, Mahakama, na umma, na kwa kuongozwa na jukumu azizi ambalo kila mwananchi wa Tanzania kupitia Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania TLS inatamka:

Tamko:

Ugonjwa wa korona upo nchini, ni wa hatari, hauna dawa rasmi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huu vimeongezeka katika miezi ya karibuni huku familia na taasisi mbali mbali, ikiwemo TLS, zikipoteza wafanyakazi, wanachama, ndugu, jamaa, majirani, na rafiki zao wengi. Ni kwa misingi hiyo kila mmoja wetu lazima achukue tahadhari zote dhidi ya ugonjwa huu kwa mujibu wa maelekezo wataalamu wa afya ili kuhifadhi haki ya kuishi ya kila mtu;

Serikali inalo jukumu kubwa la kuuongoza umma wa Watanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu wa korona na inapaswa itamke wazi kuhusu uwepo  wa wimbi la pili la ugonjwa wa korona nchini na hatua za kisayansi zipaswazo kuchukuliwa na kila mtu;

Serikali na viongozi wa umma wanapaswa wasimamie kwa ukamilifu matakwa ya ibara ya 14 na 18 za wa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Ibara ya juu ya haki ya kuishi na kuwapatia wananchi haki yao ya kupata habari na taarifa muhimu zenye manufaa kwa umma na maisha ya watu wote.

Wito kwa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania:

Mahakama zetu zijitahidi kuendesha kesi nyingi kwa njia ya mtandao;

Mahakama ziongeze wigo wa kutoa dhamana kwa watuhumiwa wenye makossa yanayodhaminika ili kupunguza misongamano ya mahabusu  katika magereza;

Mahakama zitoe adhabu ya kifungo cha nje, faini au adhabu ya kufanya kazi za jamii kwa watu watakaotiwa hatiani kuhusuna na makosa yote ambayo sheria inaruhusu adhabu hizo kutumikia ili kupuunguza msingamano wa wafungwa magerezani;  naMahakama iharakishe usikilizaji wa rufaa na mashauri ya jinai kwa na kutolea uamuzi kwa muda mfupi ili kupunguza  muda wa kukaa mahabbusu kwa watuhumiwa ambao hawatatiwa hatiani.

Wito kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania:Bunge lihiimize Serikali kuleta muswada wa marekebisho ya Sheria ya Afya ya Jamii ili kuipa tija na nguvu zaidi na kuifanya iweze kutumika kikamilifu  kupambana na magonjwa ya milipuko na pia kuwawezesha Maafisa Afya ya Jamii pamoja na Waziri wa Afya kuongoza mapambano dhidi ya magonjwa ya maangamizi; na

Bunge litoe maelekezo kwa Serikali kuwasilisha taarifa rasmi za hali ya magonjwa ya mlipouko na takwimu sahihi juu mwenendo, wagonjwa, vifo, waliopona na hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwemo kuboresha bajeti ya Wizara ya Afya.

Wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania:

Viongozi na wafanyakazi wa Serikali wachukue hatua na tahadhari za kujilinda wawapo kazini na katika mikutano. Uvaaji wa barakoa kwa usahihi iwe ni kwa wote na katika mikusanyiko yote yaani ya kiserikali na isiyo ya kiserikali. Kauli mbiu yetu iwe: vaa barakoa, barakoa, barakoa; 

Viongozi na wafanyakazi wa seka za umma na binafsi wahakikishe kuwa watu wote wanaotembelea ofisi za umma au maeneo yote ya huduma kwa umma wananawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara na kabla ya kuingia katika ofisi au sehemu yoyote ile ya huduma na pale wanaporudi nyumbani;

Taasisi za umma zinazosimamia usafiri zidhibiti misongamano ya watu katika mabasi ya umma kama vile daladala na kupigwa marufuku misongamano yote ya namna hiyo, wasafiri wote lazima wavae barakoa na kuwe na ukaaji unaozingatia umbali;

Taasisi za umma zinazosimamia michezo na shughuli za kiutamaduni zidhibiti misongamano katika michezo. Kuwepo na udhibiti mkali sana wa mashabiki na ikiwa ni pamoja kuzuia watazamaji katika michezo hadi hali itakapotengamaa;

Serikali inunue vifaa tiba vya ugonjwa huu ikiwemo mashine za okisijeni (hewa safi);

Serikali ihakikishe kuwa madaktari, wauguzi na wote wanaowahudumia wagonjwa wa virusi vya korona wanapewa nguo na vifaa vya kutosha vya kujikinga na maambukizi;

Serikali iweke utaratibu wa kuwaarifu Watanzania juu ya hali ya ugonjwa na kurudia mfumo wa kupima na kueleza idadi ya wagonjwa nchini;

Serikali isiwatie mashaka wananchi juu ya chanjo zilizotengenezwa na ambazo tayari zinatumika kuwachanja raia wa nchi nyingine bila kuwa na uthibitisho wowote ule juu ya madhara yake;

Serikali ianze mchakato wa kuchunguza chanjo zilizokwishwa tengenezwa na zinazotumiwa na nchi nyingine na kubaini zipi zinafaa kutumika nchini, kuzinunua na kuanza zoezi la kutoa chanjo kwa Watanzania wote kwa zile ambazo zitaonekana hazina madhara;

Serikali ianze kubaini shughuli zinazoweza kusambaza ugonjwa na kuzidhibiti na kuweka utaratibu wa kuziratibu;

Serikali isimamie na kutumia wataalamu wake kujifunza uzoefu wa nchi nyingine juu ya hatua walizotumia na wanazotumia kukabiliana na wimbi la pili la ugonjwa wa korona;

Serikali na viongozi wa umma waache kuwaandama na kuwasakama viongozi wa dini na kisiasa wanaosema juu ya kuwepo kwa wagonjwa wa korona na wanaotaka kuchukuliwa kwa hatua madhubuti za kupambana na ugonjwa huu;

Serikali ipitishe mwongozo wa kuwahimiza waajiri waweke utaratibu wa wafanyakazi wao kufanya kazi wakiwa majumbani kwa shughuli zile ambazo zinaweza kufanywa wafanyakazi wakiwa nyumbani ili kupunguza kuparaganyika kwa uchumi nchini;

Ugonjwa wa korona usigeuzwe kuwa hoja ya kisiasa au kuwa ni ya mtazamo upi wa kisiasa. Aidha isingeuzwe kuwaita wale wanaosema kuwa ugonjwa upo kuwa si Wazalendo. Uzalendo wa kweli ni ule unaolenga kuwakinga na kuwaponya Watanzania na si kuwaaminisha kuwa ugonjwa haupo wakati upo na unaua wananchi wenzetu na wapendwa wetu.

Wito kwa Vyombo vya Habari katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania:

Kila mwanahabari ana wajibu na haki ya kutafuta taarifa, kupokea taarifa na kusambaza taarifa sahihi juu ya ugonjwa wa korona na kueneza ujumbe wa kuwahimiza wananchi kupambana na korona bila kurudi nyuma;Vyombo vya habari viibue taarifa mbalimbali na kutoa fursa kwa wataalamu wa afya kufika katika vyombo vyao ili kuwa na mijadala huru, wazi, na ya kitaalamu juu ya mbinu za kupambana na ugonjwa wa korona;

Vyombo vya habari vitoe jumbe za kuwaelimisha wananchi juu ya mbinu za kupambana na korona na kuwahimiza wananchi kuchukua hatua za kujikinga na korona ikiwemo uvaaji wa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni; na

Kila mwanahabari, viongozi wa umma na wananchi kwa jumla wajitahidi kuheshimu tafiti za kisayansi za wataalamu wa Kitanzania na kuziwianisha na tafiti za watalaamu wa sayansi wa nchi nyingine. TLS inapenda kukumbusha kuwa pale sayansi inapouuzwa Maisha ya watu huwekwa hatarini. Mfano mmojawapo ni jinsi ambavyo Raisi Mstaafu king’ang’anizi wa Marekani, Donald Trump, alivyopuuza sayansi na kusababisha nchi hiyo, tajiri kushinda zote duniani kukumbwa na dhahama kubwa ya ugonjwa huu. Maisha ya watu wengi huko Marekani yamepotea kutokana na kupuuzwa kwa sayansi. Wataalamu wetu wa afya ya jamii na madaktari wapewe nafasi ya kueleza bila kificho hali ya ugonjwa, changamoto wanazokumbana nazo, na mafanikio yanayopatikana;Wito kwa Taasisi za Dini katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Viongozi wa kidini wachukue hatua madhubuti za kuwakinga waamini wao ikiwa ni pamoja na kuwahimiza waumini na waamini wao kufuata kanuni za afya za kupambana na wimbi hili la pili la ugonjwa wa korona;

Viongozi wa dini wawe wa wazi na wazungumze bila kificho juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa korona nchini na waziheshimu dhamira zao za ndani huku wakiwahimiza wananchi kuchukua hatua sahihi dhidi ya magonjwa ya mlipuko kama korona; na

Kipindi hiki cha Kwaresma tulichomo na kile cha Ramadhani, kinachofuata mara baada ya Kwaresma, vitumike kutubu na kumuomba Mungu wetu Mwema atuonee huruma na kutuponya sisi na dunia nzima na ugonjwa huu.

Wito kwa Watu Wote katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania:

Kila mtu ajitahidi kuendelea kutumia uzoefu wa kupambana na korona tulioupata mwaka jana ikiwa ni pamoja na kujifukiza, kufanya mazoezi, kujikinga kwa kuzingatia umbali wa mita mbili  na kati ya mtu na mtu na kuvaa barakoa;

Kila mtu ajitume katika kufuata miongozo ya afya ya jamii iliyotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni;

Waajiri wengi wawaweshe wafanyakazi wao kufanya kazi kutokea nyumbani kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa majumbani na waweke utaratibu mzuri wa kuwalinda wafanyakazi wao wanaolazimika kwenda kazini kila siku;

Kila mtu achukue hatua za kujikinga na ugonjwa wa korona ikiwemo kuvaa barakoa, umbali wa kijamii, kunawa kwa sabuni na maji tiririka, na kufanya mazoezi; na pia kila mtu achukue hatua hizo kuwalinda wengine hasa makundi tete wakiwamo wazee, watu wenye ulemavu, watoto, wajawazito na wagonjwa;na

Kila mtu afahamu kuwa uhai wake alipewa na Mungu na si serikali au kiongozi yeyote yule hivyo ana jukumu la kuulinda. Aidha, kila mtu ana jukumu la kupima kwa makini kauli zinazotolewa na watu au viongozi juu ya njia sahihi za kupambana na ugonjwa wa korona. Kila mara tukumbuke msemo wa Raisi Kikwete kuwa “akili za kuambiwa changanya na za kwako;”

TLS inaamini kuwa hatua hizo hapo juu na nyingine ambazo zimependekezwa na taasisi nyingine (ikiwemo MAT) na watu wengine wanaokiri kuwepo kwa ugonjwa huu zikichukuliwa kwa haraka na kutekelezwa kwa makini nchi yetu itaushinda ugonjwa huu.  Uzoefu wetu wa mwaka jana ni mkubwa tuutumie kwa makini. Aidha, tusisahau kuwa “kinga ni bora kuliko tiba” na hatua za kujikinga zipewe kipaumbele cha kwanza. Uvaaji wa barakoa uwe wa lazima na si hiari tena.

Mwisho, TLS inawataka Watanzania wote kushikamana na kuendesha mapambano dhidi ya korona kwa pamoja. Watanzania tuone kuwa kuumwa kwa mmoja wetu ni kuumwa kwetu sote na hivyo tushirikiane katika kumuokoa kila mmoja wetu. Tusibaguane na kuyafanya mapambano dhidi ya ugonjwa huu kuwa ya kisiasa au tofauti za kiitikadi na kimtazamo.

Mungu ibariki Tanzania na Mungu iponye Tanzania na Dunia Nzima.

Imetolewa jijini Dar es Salaam Kwa Amri ya Baraza la Uongozi wa TLS  Dar es Salaam leo tarehe 18 Februari  2021.

Dkt. Rugemeleza A.K. Nshala

RAISI

Tamko-la-TLS-juu-ya-Wimbi-la-Pili-la-Mlipuko-wa-Ugonjwa-wa-Korona-2021

Leave a Comment

Calendar
August 2022
M T W T F S S
1234567
891011121314
15161718192021
22232425262728
293031  

Get In Touch

Latest Posts

Shopping Cart

No products in the cart.