Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanzania Bara (TLS) limepokea taarifa za kukamatwa na kushikiliwa kwa mwanachama mwenzetu na baadhi ya vyombo vya dola kwa mahojiano. Mwanachama huyo ndugu MANENO MBUNDA, mwenye namba ya uwakili 5902 ni mwajiriwa wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na pia yupo chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu na Wakili Mkuu wa Serikali.

Baraza la Uongozi kwa kushirikiana na Uongozi wa Ofisi ya TLS ya Kanda ya Arusha tangu lilipopata taarifa ya kukamatwa kwake limefuatilia na linaendelea kufuatilia kwa ukaribu na umakini  sana suala hili.  Vilevile Baraza liliwasiliana na linaendelea kuwasiliana na mamlaka zote husika ili kujua sababu za kushikiliwa kwa Wakili Maneno  Mbunda ili kuweza kuchukua hatua zinazopaswa katika kutetea na kulinda haki zake kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Baraza la Uongozi wa TLS linazikumbusha  mamlaka zote za serikali kuheshimu na kufuata kwa ukamilifu matakwa yote ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na sheria za nchi. Moja ya matakwa hayo ni pamoja na kutomshikilia  mtu yeyote yule kwa zaidi ya saa 24, na kutomhoji kwa kificho, kutomtesa, kutomtisha na kumuhoji pasipo kuwa na huduma ya wakili au mwanafamilia wake.

Baraza la Uongozi wa TLS linawaomba wanachama wake kuendelea kuwa watulivu wakati huu linapofuatilia suala hili kwa ukaribu na umakini mkubwa. Pia Baraza litaendelea kuwafahamisha na kuwapa  taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana na hatua zitakazochukuliwa katika kufikia hitimisho la suala hili.

Mwisho, Baraza la Uongozi linaishukuru familia ya Wakili Maneno Mbunda na baadhi ya wanachama wa TLS kwa kutoa taarifa mapema na kuliwezesha kufuatilia suala hili kwa ukaribu tokea liliporipotiwa hadi wakati huu linapotoa taarifa hii ya awali.

Wenu

Dk. Rugemeleza A.K. Nshala

RAIS

PDF File ==>TAARIFA YA KUKAMATWA WAKILI MBUNDA (1)

You may also like

Leave A Comment

Please enter your name. Please enter an valid email address. Please enter message.