Jumuiya ya Wanasheria Tanganyika (TLS) ni jumuiya ya wanataaluma wa sheria wa Tanzania Bara iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 307 ya mwaka 1954. Kazi kuu ya jumuiya hii ni pamoja na kutetea na kulinda na kuboresha mazingira ya kazi ya wanataaluma wa sheria, kutoa ushauri wa masuala ya kisheria kwa serikali na mahakama  pamoja na kuusaidia umma wa watanzania katika masuala yote  yanayohusu sheria.

Kwa niaba ya Baraza la Uongozi la TLS napenda kuipongeza serikali, hususani Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi na Utawala Bora na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  muongozo walioutoa katika Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge  tarehe 15/04/2019 wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi na Utawala Bora akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake.

TLS inaipongeza  Serikali kwa kutoa muongozo huo na  kukemea vikali viongozi wa Serikali hususani baadhi ya Wakuu wa  Mikoa na Wilaya ambao kwa muda mrefu, licha ya maelekezo ya serikali, wamekuwa  wakitumia madaraka yao vibaya bila kufuata taratibu za kisheria kwa kuwakamata na kuwaweka wananchi kizuizini. Aidha, pamoja na kuwepo kwa muongozo wa kisheria, TLS inampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa waraka na kuusambaza kwa wahusika wote kama ilivyonukuliwa toka kwenye majibu ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi na Utawala Bora, Ndugu George Mkuchika. Wito wetu kwa Mwanasheria Mkuu ni kumtaka kuusambaza waraka huo kwa  vyombo vya habari na wananchi ili wananchi wote waufahamu na waweze kuhoji pale madaraka yanapotumika vibaya.

Kwa muda mrefu sana TLS na wananchama wake wamesikitishwa sana na mwenendo huo wa baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Wilaya na hata baadhi wa watumishi wa Serikali hususani Jeshi la Polisi kwa kutumia madaraka yao vibaya na kuwaweka kizuizini wananchi na mawakili kinyume na utaratibu uliowekwa na sheria. Vitendo hivyo ni uvunjwaji wa Katiba na Sheria za nchi yetu kwani havitokani na mtu au wakili kuwa ametenda kosa bali kwa lengo la kuwakomoa, kuwatisha, na kujikuza.

TLS inathamini uhusiano bora na taasisi zote za Serikali lakini haitasita kuwataka wanachama wake na wananchi kuwashitaki viongozi wa serikali ambao wanakiuka sheria ikiwa ni pamoja na kuwaweka ndani mawakili na wananchi ambao hawajafanya kosa lolote lile la jinai wala kuhatarisha amani. TLS inasisitiza kuwa Katiba ya nchi yetu inatoa hakikisho la watu kuwa huru na kuwa uhuru huo tu unaweza kuingiliwa pale mtu anapokuwa ametenda kosa la jinai na si vinginevyo. Utawala wa sheria unadai kufuatwa kwa sheria na watu wote ikiwemo viongozi wote wa serikali. Viongozi na polisi wetu, kwa kweli, ndio ambao wanatakiwa kuwa mfano wa kufuata sheria. Kufuatwa kwa sheria hujenga imani kubwa sana kwa serikali, mahakama, na bunge na huchagiza utawala bora ikiambatana na ustawi wa nchi kiuchumi, kijamii, na kisiasa. Ubabe huondoa imani ya wananchi kwa serikali, mahakama, na bunge lao.

Aidha tunaipongeza serikali kwa kuwakumbusha viongozi wote kuheshimu msingi wa kikatiba wa utengano wa mamlaka na kutokuingiliana kwa mihimili ya serikali (separation of power). Tunasema kuwa muhimili pekee wenye Mamlaka ya kuamua migogoro baina ya watu au watu na serikali ni mahakama na si wakuu wa Mikoa au wa Wilaya. Hivyo kesi zikishapelekwa mahakamani ni mahakama pekee ndiyo yenye kauli ya mwisho juu ya kesi hizo na si kiongozi yeyote yule wa serikali. Na kama kesi ikiamuriwa na mtu au kiongozi hajaridhika anayo haki ya kukata rufaa kwa mahakama ya juu ya ile iliyoamua hadi kufikia Mahakama ya Rufaa. TLS haitakaa kimya pale ambapo msingi huu unakiukwa na inawataka wananchi kutokaa kimya bali kuchukua hatua zipaswazo dhidi ya wote wanaokiuka sheria za nchi zetu eti kwa vile ni wakuu wa mikoa au wilaya.

Mwisho, tunashauri Ofisi ya Raisi na Utawala Bora pamoja na Mwanasheria Mkuu zitoe mafunzo ya misingi ya sheria na katiba kwa viongozi na watumishi wa umma na juu ya kufanya kazi kwa kuzingatia msingi wa utawala bora na Uhuru na utegemeanaji wa mihimili ya dola. TLS kama ilivyonawajibu wa kuishauri serikali, tunapenda kueleza wazi tuko tayari kushirikiana na ofisi hizo mbili na ofisi zingine za serikali katika kutoa mafunzo hayo lakini pia katika kuhakikisha utawala wa sheria unafuatwa hapa nchini na haki haswa kwa wananchi wa kipato cha chini inapatikana kwa wakati.

Signed doc==> Pongezi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Utawala Bora na Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Limetolewa Jijini Dar es Salaam leo tarehe 18 Aprili 2019.

RUGEMELEZA A.K. NSHALA

RAISI- TLS

You may also like

Leave A Comment

Please enter your name. Please enter an valid email address. Please enter message.